Chid Benz kupumzishwa na 20 kali
KABLA ya kupumzika kujishughulisha na muziki wa kizazi kipya, Chid Benz amesema atatoa nyimbo zaidi ya 20 zitakazoweza kufanya vizuri hata baada ya hatua yake hiyo
Akizungumza na mtandao huu mapema wiki hii, Chid alisema kuwa kabla ya kuachana na muziki kwa lengo la kufanya mambo yake ya kifamilia anatarajia nyimbo hizo zitakuwemo katika albamu yake mpya ambayo ataizindua Mei mwaka huu.
Chid alisema kuwa licha ya kujiweka katika mapumziko ya mambo ya muziki, ana uhakika wa kuendelea kusikika katika vyombo vya habari kwa kipindi kirefu kutokana na ubora wa nyimbo zitakazokuwa zikitoka kila wakati.
“Nina nyimbo zaidi ya 20 ambazo naziandaa, hata kama nikiachana na muziki kwa kipindi cha miaka kumi lakini nina uhakika wa nyimbo zangu kutesa katika vituo mbalimbali vya redio na luninga kutokana na ubora na ujumbe uliomo ndani yake,” alisema Chid.
Mbali ya kutingwa na masuala ya kifamilia, Chid anatarajiwa kukitumia kipindi cha mapumziko yake kwa kujiendeleza kielimu kutokana na elimu aliyonayo kutokidhi mahitaji.
Post a Comment