Serikali yawakemea Mengi na Rostam
SERIKALI imetoa tamko rasmi kubeza malumbano yaliyoibuka hivi karibuni kati ya Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na mfanyabiashara mwenzake, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, alisema serikali inawataka Mengi na Rostam, kuacha mara moja malumbano yao kupitia vyombo vyao vya habari wanavyovimiliki na badala yake wawasilishe madai na vielelezo vyao kwa mamlaka husika ili hatua zinazofaa zichukuliwe.
Akisoma tamko hilo lililosainiwa na Waziri wa wizara hiyo, Kapteni mstaafu George Mkuchika, aliyeko Busanda, wilayani Geita, mkoani Mwanza, kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mdogo, alisema uchunguzi walioufanya na vyombo vya dola, umebaini kuwa Rostam na Mengi, wamekiuka sheria kwa kutumia vyombo vyao vibaya na wanaweza kuligawa taifa.
“Serikali imetafakari kwa makini malumbano ya wafanyabiashara hawa na kubaini kuwa wanalipeleka taifa pabaya, kwani malumbano yao yanaweza kuligawa taifa na kutishia uvunjifu wa amani, kama yataachwa yaendelee.
“Serikali imebaini kuwa malumbano ya Mengi na Rostam, yamewagawa wananchi katika makundi mawili, ya wale wanaounga mkono kauli za Rostam na wanaomuunga mkono Mengi,” alisema Naibu Waziri Bendera.
Bendera alienda mbali kwa kusema kuwa malumbano hayo, yamesababisha kuwapo kwa matumizi mabaya ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Mengi (redio, magazeti na televisheni), na Rostam, ametumia vibaya magazeti yake, kwa manufaa binafsi, kinyume cha maelekezo ya sera ya habari na utangazaji ya mwaka 2003.
“Sera ya habari ya mwaka 2003, imekataza chombo cha habari kutumika kwa manufaa binafsi ya mmiliki au mtendaji, bali kitumike kwa manufaa ya umma, chombo cha habari kiongozwe na maadili ya taaluma na jamii husika na chombo cha habari kisitangaze habari kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, kabila, dini, jinsia, au ulemavu au kuchochea uhasama.
“Kwa hali hiyo, malumbano ya Rostam na Mengi yakiachwa yaendelee, yanaweza kulitumbukiza taifa pabaya katika uvunjaji wa amani,” alisema.
Alionya kuwa serikali haitakubali kusikia malumbano ya Rostam na Mengi, ambayo yanaweza kuhatarisha hali ya utulivu na amani nchini yakiendelea bila sababu za msingi.
“Serikali pia haitavumilia kuona vyombo vya habari nchini vikichangia kuligawa taifa katika makundi na kudumaza maendeleo,” alisema.
Aliwataka Rostam na Mengi, kukumbuka kuwa malumbano yao kwa kutumia vyombo vyao vya habari na wakati mwingine kuonekana kana kwamba wanalihutubia taifa, ni kutowatendea haki watu wengine ama kampuni au mashirika ambayo yametajwa katika malumbano hayo lakini hawana vyombo binafsi.
“Hawa wengine wameonewa, hawana vyombo vya habari, unanitaja mimi Bendera, sina gazeti, nitatumia nini kuzungumzia? Nitajielezea wapi kama walivyotumia Rostam na Mengi?” alihoji Bendera.
Naibu waziri huyo alizidi kueleza kuwa serikali inasikitishwa na kitendo cha Mengi cha kuzungumzia kesi ambazo tayari zipo mahakamani wakati sheria za nchi zinakataza mtu, watu, kuzungumzia ama kujadili suala ambalo lipo mahakamani, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwahukumu na kuwatia hatiani wahusika bila wao kupewa fursa ya kujitetea au kusikilizwa.
“Serikali inawataka wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini katika kutimiza wajibu wao kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao badala ya kuandika au kutangaza kulingana na matakwa ya wamiliki wa chombo husika,” alisema.
Hata hivyo Naibu Waziri hakuweza kujibu maswali ya wanahabari kwani kila alipoulizwa swali, alitoa majibu ya mkato na kudai kuwa huo ndio msimamo wa serikali na taarifa yake inajitosheleza.
“Hii taarifa ni msahafu tosha, kila kitu kipo hapa, someni mstari kwa msitari, tumefanya uchunguzi wa kitaalamu,” alianza kuwaeleza waandishi wa habari kabla ya kuuliza maswali.
Alipoulizwa kuhusu uhalali wa Televisheni ya Taifa (TBC1) kurusha kipindi maalumu cha Rostam, wakati alitumia nafasi hiyo pia kumsema Mengi kwamba alitumia kituo chake cha ITV vibaya, Bendera aliruka kwa kusema hiyo si kazi yake, bali ya Bodi ya TBC1 na ndio wanaopaswa kuulizwa na kujibu swali hilo.
“Mimi si msemaji wa TBC1, kuna Tido na bodi yake, kawaulize kama Rostam alikuwa sahihi au alikosea,” alisema waziri huyo kwa ufupi.
Alienda mbali zaidi na kusema kuwa kuanzia sasa serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa vyombo vya habari ambao hawatazingatia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na sheria ya utangazaji ya mwaka 2003 katika kutekeleza kazi zao za kukusanya na kusambaza habari.
Alipoulizwa ni kwanini serikali isitunge sheria ya kukataza viongozi wa umma, kama wabunge kumiliki vyombo vya habari, alisema serikali haijachelewa bado kwani inaweza kufanya hivyo ikiona inafaa.
Tamko hilo la serikali kupitia wizara hiyo limekuja wakati yalishatolewa matamko mengine mawili kwa nyakati tofauti na viongozi wa juu wa serikali.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikwisha kutoa msimamo wa serikali alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo mjini Dodoma wakati wa mkutano wa 15, akiwataka waliokashifiwa na Mengi kwenda mahakamani, huku vyombo husika vikichunguza tuhuma hizo.
Mbali na Pinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba, alishatoa msimamo wa serikali, kwa kusema Mengi amechemka kuwataja wenzake mafisadi papa, kwani hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Hata hivyo, Waziri Bendera alisema kauli aliyoitoa ndio msimamo unaotambuliwa na serikali na si vinginevyo.
“Nimesema, msemaji wa serikali ni mimi, wizara yangu ndiyo yenye mamlaka ya kuzungumzia lolote linaloigusa serikali, taarifa yangu ndiyo inayopaswa kuzingatiwa,” alisema huku akionyesha karatasi zake juu na kuongeza kuwa:
“Hii ndiyo taarifa ya serikali, waziri wangu yupo makini, tunakwenda kwa data (takwimu), tuna watu weledi na wataalamu, vingine hatuvitambui,” alisema.
Pia naibu waziri hakuweza kuwaeleza wanahabari sababu za kuzungumzia suala hilo, hasa la kuchafuana kati ya wafanyabiashara hao wawili, wakati tayari walishapelekana mahakamani kwa kesi hiyo hiyo, na kudai kuwa serikali haikurupuki na haijachelewa kutoa tamko lake.
“Serikali haikurupuki, na haifanyi kazi kwa kuendeshwa na watu, haijachelewa kutoa tamko hili,” alisema naibu waziri bila kufafanua.
Aidha, swali jingine ambalo waziri hakutaka kulijibu ni lile lililohusu tuhuma za ufisadi zilizowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilibrod Slaa, aliyetaja majina ya watu 11, mwaka 2007.
Swali hilo lilitaka kujua kwanini serikali haikutoa tamko badala yake ikawachunguza kimya kimya watuhumiwa na baadhi yao kufikishwa mahakamani, lakini kwanini tuhuma alizotoa Mengi zinapaswa kutolewa vielelezo na ushahidi?
Tuachane na mambo ya zamani, tuangalie yaliyopo leo,” alimalizia Waziri Bendera na kuondoka huku waandishi wa habari wakinung’unika kwa baadhi ya maswali yao ya msingi kutopewa majibu ya kuridhisha.
Wakati serikali ikitoa tamko lake jana, tayari Mengi amekwisha kumshitaki Rostam kwa kumkashifu, akitaka amlipe sh bilioni 10, huku Rostam akiwa amepeleka vielelezo vyake dhidi ya Mengi katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakati Manji amekimbilia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mahakama ya Kisutu, akilalamika kukashifiwa na anadai kulipwa fidia ya sh moja.
Naibu waziri alihitimisha kwa kusema kuwa serikali kwa mara nyingine inasisitiza kuwa malumbano dhidi ya ufisadi na vitendo vya rushwa bado yanaendelea na inawahimiza wananchi wenye taarifa za vitendo kama hivyo watoe taarifa kwenye vyombo vya dola.
Malumbano hayo yalianza pale Mengi alipoitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwataja wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia kuwa ni ‘mafisadi papa’, wanaolifilisi taifa.
Mengi aliwatuhumu wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia, Jeet Patel, Rostam Aziz, Yusuf Manji, Subhash Patel, na Tanil Sumaiya kuwa ni mafisadi papa wanaoliibia taifa mabilioni ya fedha.
Mbunge wa Igunga, Rostam, ndiye alikuwa wa kwanza kujibu tuhuma hizo, lakini naye alimtuhumu Mengi kuwa ni fisadi nyangumi kwa kumhusisha na kukopa fedha za Mpango wa Kusaidia Wafanyabiashara - Commodity Import Support (CIS).
Juzi mfanyabiashara mwingine Shubhash Patel, aliyetuhumiwa na Mengi kuwa miongoni mwa mafisadi papa, alijitokeza na kudai kuwa Mengi amemkashifu, lakini hajaamua endapo atakwenda mahakamani.
Source: Tanzania Daima
Post a Comment