Rais Obama Akimbizwa Mafichoni baada Ndege Mbili Kutinga Anga ya Ikulu


Rais Barack Obama na makamu wake Biden walichukuliwa na kufichwa mafichoni ndani ya ikulu ya Marekani kwa kipindi kifupi baada ya ndege mbili ndogo kukatiza mipaka na
kuingia kwenye anga ya ikulu jijini Washington.
Maafisa wa ulinzi ndani ya White House waliwaondoa watalii na watu wote waliokuwa nje ya majengo ya ikulu.

Ndege zote mbili zilivunja mipaka ya anga iliyowekwa karibu na ikulu na kukatiza katika eneo ambalo ndege huwa haziruhusiwi kupita.

Hatua hiyo ilileta hofu na kukumbushia mkasa wa septemba 11 mwaka 2001 ambapo ndege za magaidi ziligonga jengo la Pentagon, majengo ya World Trade towers jijini New York na ndege moja kudondoka kwenye viwanja vya Pennsylvania.

Rais Obama na makamu wake wa rais Biden walifichwa kwa muda katika maficho ambayo msemaji wa White House Robert Gibbs hakutaka kuyataja.

Gibbs alisema kwamba tukio hilo lilikuwa la muda mfupi sana na Obama na watu waliokuwemo ndani ya ikulu waliendelea na kazi zao baada ya ndege hizo kuonekana sio tishio na kuondolewa maeneo ya ikulu.

Helikopta mbili za ulinzi na ndege mbili za kijeshi Air Force F-16 zilitumwa kuziongoza ndege hizo kuelekea nje ya mipaka ya anga ambayo ndege zingine huwa haziruhusiwi kupita.

Taarifa zilisema kwamba marubani wa ndege hizo mbili walikuwa hawajuani na walikuwa wakielekea sehemu tofauti.



0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2009 Bloggerized by : CTU | Inspired By ReedzSolution : ReedzSolution