Jacob Zuma juu zaidi

Sasa ni miujiza tu itamfanya Jacob Zuma wa chama tawala cha African National Congress (ANC), asiingie ikulu ya Afrika Kusini kama rais wa nne mweusi wa taifa hilo lenya nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika, baada ya ushindi wa kishindo aliokwisha kujikusanyia.

Katika kura zilizokwisha kutangazwa si tu kwamba Zuma maarufu kwa jina la JZ anaongoza kwa mbali, bali anaelekea kupata ushindi wa zaidi ya theluthi mbili ya kura, tofauti na makadirio ya awali.

ANC ina zaidi ya kura milioni 12 ambazo zimeshahesabiwa, ambayo ni sawa na asilimia 67.2.

Chama cha Democratic Alliance (DA) kinashikilia nafasi ya pili kwa kupata asilimia 16 na Chama kipya cha Congress of the People (Cope), kilichojimega kutoka ANC kwa ghadhabu za kuenguliwa madarakani Rais Thabo Mbeki, kina asilimia 7.6.

Matokeo kutoka maeneo yanayokaliwa na weusi wengi, ikiwemo Soweto bado yanasubiriwa. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa leo.

Matokeo hayo yanaipa ANC theluthi mbili ya kura zote, Lakini ilikuwa mbele kwenye majimbo manane kati ya tisa nchini. Asilimia 80 ya waliotarajiwa kupiga kura walijitokeza kupiga kura Jumatano wiki hii.

Usiku wa kuamkia jana, Mwenyekiti wa ANC, JZ, aliueleza umati wa wafuasi wake kuwa ushindi huo ni imani ya wananchi kwa chama chao. JZ aliungana na maelfu ya wafusi wa ANC kusherehekea mjini Johannesburg ushindi wa chama hicho ambao unamsimika kuwa rais wa taifa lenye uchumi na ushawishi mkubwa kidiplomasia duniani.

JZ bingwa wa kuhasisha umma, alikuwa akicheza na kuimba wimbo maalum uliokuwa ukitumika wakati wa ukombozi kutoka kwa makaburu wa 'nipe silaha yangu'.

``Chama hiki ni tembo. Huwezi kushindana na tembo,`` alisema JZ akishangiliwa na wafuasi wa ANC, waliojipamba na mavazi ya rangi za njano, kijani na nyeusi.

``Huhitaji theluthi mbili kuongoza nchi. Unahitaji utashi wa kisiasa kufanya hivyo,`` alisema msemaji wa ANC, Jessie Duarte.



0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2009 Bloggerized by : CTU | Inspired By ReedzSolution : ReedzSolution