Wabunge wamuunga Mengi mkono dhidi ya...

Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Wilibrod Slaa, amepongeza hatua ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, kuwataja kwa majina hadharani, watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi akisema ni ujasiri ambao wananchi wengi wenye uchungu na nchi wanapaswa kufuata nyayo hizo.

Akizungumza na Nipashe nje ya viwanja vya Bunge hapa mjini Dodoma jana, Dk. Slaa alisema: ``Nina gazeti hapa (la Nipashe), lakini sijalisoma kwa undani na hivyo siwezi kutoa maoni yangu kwa undani sana.

Hata hivyo, kitendo tu cha kwenda hadharani na kuwataja watuhumiwa, ingawa sijui vyema ushahidi uliomfikisha hapo litakapokuja suala la uthibitisho mahakamani, ni ujasiri mkubwa sana ambao mimi nina upongeza.``

Dk. Slaa alisema majina aliyoyataja Mengi ni yale ambayo hata yeye anayajua kwamba yamebobea katika ufisadi.

``Majina haya si mageni. Ni yale yale ambayo yameshatajwa kila mara kuhusika na ufisadi,`` alisema.

Alipoulizwa kama hatua hiyo ni muhimu katika kupambana na ufisadi nchini, Dk. Slaa alijibu. ``Definitely (swadakta). Hiyo ni hatua muhimu sana katika kupambana na ufisadi.

Tunahitaji raia wengi kama Mengi wajitoe mhanga kupigania nchi yetu dhidi ya mafisadi ambayo katika siku za karibuni yalianza kutumia fedha kuanzisha magazeti na kuyatumia kwa lengo la kujisafisha.``

Naye Shoka Khamis Juma, Mbunge wa Micheweni (CUF) ambaye pia ni waziri kivuli wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia utawala bora, alisema Mengi anatakiwa kuungwa mkono kwa gharama yoyote kwa sababu amefanya kile ambacho vyombo husika (polisi) wameshindwa kufanya.

Alisema kama mbunge anayehimiza utawala bora, sambamba na wabunge wengine wanaoamini katika hilo, wanamuunga mkono Mengi.

Alisema kundi la mafisadi-papa limekuwa likiwaumiza sana Watanzania kutokana na rushwa ambayo inawaongezea umaskini wananchi na kwamba hatua ya Mengi ni muhimu sana, kwani pia inachangia harakati za wabunge wa upinzani na wale wa CCM wanaochukia ufisadi katika kuindolea nchi tatizo hilo.

``Tusamaki tudogo tudogo nditwo tumekuwa tukitajwa (samaki wadogo wadogo ndio wamekuwa wakitajwa), lakini mapapa haya ndio hatari zaidi. Yanapaswa yatajwe hadharani na huu ndio uzalendo,`` alisema na kuongeza ``Hongera Mengi, sisi tutashirikiana nawe kupambana na ufisadi.``

Akiongea huku akiwa na wabunge wenzake watatu baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mbunge Juma alisema, China inafanya maendeleo makubwa kwa sababu haina utani na mafisadi (kwani sheria zao hutoa adhabu ya kifo).

Alisema ukimya limekuwa si jambo la kusaidia na kilichokuwa kinatakiwa ni kuwataja watuhumiwa hadharani kama alivyofanya Mengi na kwamba hakuna sababu ya kuwaonea aibu mafisadi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam juzi, Mengi alisema nchi inapata matatizo mengi kutokana na rushwa kubwa kubwa zinazofanywa na mafisadi-papa.

``Mafisadi wote na hasa wale wanotuhumiwa kuwa mafisadi-papa ni lazima washughulikiwe, la sivyo watayumbusha na kutingisha nchi yetu. Ni lazima tuone sasa tumefika mahali pa kusema inatosha,`` alisema.

Aliwataja watuhumiwa watano kati ya aliyosema hawazidi 10 kuwa ni Rostam Aziz, Tanil Somaiya, Yusuf Manji, Jeetu Patel na Subash Patel.



0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2009 Bloggerized by : CTU | Inspired By ReedzSolution : ReedzSolution