Madaraja mikopo Elimu ya Juu kuongezwa

KUANZIA mwaka ujao wa fedha Serikali itaongeza madaraja ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kutoka matano ya sasa na kufikia 11

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Bw. Mizengo pinda alisema hatua hiyo imelenga kutoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kupata elimu chini ya utaratibu huo.

Alisema utaratibu wa sasa uligawa makundi hayo katika madaraja matano ambapo Kundi la A lilipewa mkopo wa aslimia 100, Kundi B asilimia 80, Kundi C asilimia 60, Kundi D asilimia 40 na Kundi E asilimia 20.

Kunzia mwaka ujao wa fedha, 2009/10 Serikali itaongeza madaraja hayo ambapo kundi A litapata mkopo wa asilimia 100, Kundi B asilimia 90, Kundi C asilimia 80, Kundi D asilimia 70, Kundi E asilimia 60, Kundi F asilimia 50, Kundi G asilimia 40, Kundi H asilimia 30, Kundi I asilimia 20,Kundi J asilimia 10 Kundi J asilimia 0.

Bw. Pinda alisema Serikali itajitahidi kusimamia utaratibu huo ili kuhakikisha hauleti manung'uniko kwa wananchi.

"Tutazingatia mambo mengi ikiwa ni pamoja na hali ya mwombaji, wazazi , shughuli za kiuchumi , mali za mwombaji, wazazi, hali ya maisha ya mwombaji na hali ya kijamii ya mwombaji" alisema.

Alisema pamoja na nia njema ya Serikali kutahakikisha wanafunzi wote wenye sifa wanapata elimu ya juu chini ya utaratibu huo, bado kuna ugumu wa kutoa mikopo wa asilimia 100 kwa kila wanafunzi kutokana na matatizo ya kiuchumi.

Hata hivyo alisema sera ya uchangiaji elimu ya juu si mbaya na kuwataka wenye uwezo kuitekeleza ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wengine kupata elimu.

Akizungumzia madai ya mishahara ya walimu alisema Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kulipa madai hayo na kuahidi kuendelea kutekeleza jambo hilo hilo.

Hata hivyo alisema yamejitokeza mambo yanayochangia ulipaji madai mbalimbali ya walimu na kuyataja kuwa ni pamoja na kukosekana kwa nyaraka na viambatanisho vingine, vyeti vya ndoa na watoto, fomu za likizo, barua za uhamisho na vibali vya waajiri, vivuli vya risiti, udanganyifu wa kughushi.

Alisema Serikali itaendelea kulipa madeni hayo na kukubaliana na hoja inayotolewa na walimu kuwa matatizo yao mengine yamechangiwa na idara hiyo kuwekwa katika mamlaka mbalimbali.

Akizungumzia matokeo ya kidato na sita aliwataka walimu waliochelewesha taarifa za alama za majaribio ya wanafunzi kuhakikisha wanatekeleza jambo hilo haraka vinginevyo watachukuliwa hatua stahiki.

Hali ya chakula

Alisema taarifa zilizopo zinaonesha kuwa hali ya chakula nchi si nzuri na kuwataka wananchi kutunza chakula na kueleza kuwa Serikali itaendelea kudhibiti uuuzaji chakula nje ya nchi.

Alisema tatizo hilo limechangiwa na baadhi ya mikoa nchini kukosa mvua za vuli na hivi sasa Serikali inafanya utaratibu kusambaza mbegu mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame, mihogo na viazi.

Alitaaja baadhi ya mikoa yenye nafuu ya chakula kuwa ni pamoja na Kigoma , Rukwa Mbeya, Iringa , Morogoro, Dodoma, Singida, Manyara na Tabora.

Mikoa inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula ni pamoja na Pwani, Lindi, Mtwara na Dar es Salaam.

Alisema mtikisiko wa uchumi duniani umeathiri bei ya zao la pamba katika soko la dunia hata hivyo alisema bei za mazao mengine kama sukari, tumbaku, korosho,chai pareto zimeendelea kuwa nzuri.



0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2009 Bloggerized by : CTU | Inspired By ReedzSolution : ReedzSolution