Jacob Zuma Amchagua Mke Mkubwa Kwenye Kuapishwa Kwake.
Jacob Zuma akiambatana na mke wake mkubwa Sizakele Khumalo katika kuapishwa kwake
Jacob Zuma ameapishwa kuwa rais wa nne wa Afrika Kusini akipewa kampani na chaguo lake la kwanza katika wake zake watatu, mke wake mkubwa Sizakele Khumalo huku wake zake wadogo wakiangalia tukio hilo kwa mbali kwenye jukwaa la VIP.
Kwa viongozi wengine huenda wasingehitaji kufikiria sana ni nani wa kuambatana naye katika tukio muhimu kama hili lakini Jacob Zuma alikuwa na wakati mgumu wa kumchagua mke wake mmoja ambaye atapewa heshima ya kiserikali katika tukio hilo la kihistoria la kuapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini.
Vyombo vya habari vya Afrika Kusini kwa miezi kadhaa vilikuwa na shauku kubwa ya kufahamu mke yupi wa Zuma kati ya wake zake watatu angepata nafasi hiyo muhimu na ya kihistoria.
Alikuwa ni mke wake mkubwa Sizakele Khumalo aliyepata nafasi ya kupata heshima hiyo na kupanda na mumewe kwenye jukwaa kumpa kampani katika tukio hilo muhimu.
Bi Khumalo alimshuhudia mumewe akipiga magoti mbele ya Nelson Mandela kama heshima kwa mzee Mandela.
Wake wengine wawili wa Zuma waliachwa wamesimama pamoja kwenye sehemu ya wageni VIP wakishuhudia kwa mbali tukio hilo.
Katika hotuba yake baada ya kuapishwa mbele ya watu elfu 30 waliohudhuria sherehe hizo, Rais Zuma aliahidi kufuata nyayo za kiongozi wa zamani Nelson Mandela katika kuliongoza taifa hilo.
Chama cha African National Congress, ANC kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika tarehe 22 mwezi Aprili.
Kiongozi huyo wa chama cha ANC mwenye umri wa miaka 67 alikabiliwa na kashfa za ubakaji na rushwa mashtaka ambayo yalitupwa nje na mahakama muda mfupi kabla ya uchaguzi kufanyika.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi wengine wa mataifa mbali mbali kama vile Kiongozi wa Libya Muammar Kadhaffi na Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe.
Post a Comment