'Muuaji' asimulia walivyomchinja albino


JESHI la Polisi wilayani Bariadi mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na wanannchi wa kijiji cha Mkingwabie, wamefanikiwa kukamata kichwa na miguu miwili iliyonyofolewa kwenye mwili wa albino, Bw. Lyaku Nkanyabilu (50), aliyeuawa kikatili mjini hapo na kuzikwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Viungo hivyo vilipatikana jana nyumbani kwa Bw. Mbonje Mawe (41), mkazi wa kijiji hicho na Majira ilishuhudia polisi wakishirikiana na wananchi kufukua kichwa cha marehemu Nkanyabilu nyumbani kwa mtuhumiwa wa mauaji.

Baada ya kufukuliwa kichwa hicho, Bw. Mawe aliongoza kundi la polisi na wananchi hao kwenda sehemu iliyokuwa imefukiwa miguu ya albino huyo ambapo ilifukuliwa ikiwa imefungwa na gunia.

Bw. Mawe alikiri kushiriki mauaji hayo na kuwataja wenzake sita anaodai kushirikiana nao, akiwemo Mwenyekiti wa kijiji hicho, pamoja na wenyeviti wawili wa vitongoji. Alisema walikuwa na nia ya kuuza viungo hivyo kwa wateja ambao walikuwa wakiwasiliana.

Akisimulia tukio zima lilivyokuwa, Bw. Mawe alidai siku ya tukio akiwa na wenzake sita, walipanga kumuua Bw. Nkanyabilu kwa kushirikiana na shemeji yake, Bw. Sayi Gamani.

Alidai Bw. Gamani alimdanganya Bw. Nkanyabilu kuwa anampeleka hospitali kumtibu maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kabla ya kushirikiana kumkamata na kwenda kumuua.

"Ilipofika saa saba usiku, tulimkamata Bw. Lyaku (Nkanyabilu) na kumpeleka mtoni, tulipofika huko tulimlazimisha kuingiza kichwa kwenye maji hadi alipokufa, tukamchinja, tukamkata miguu na baada ya hapo, tukaiingiza viungo hivyo kwenye gunia moja na mwili wake kwenye gunia lingine na kutumbukiza mwili wake kwenye maji," alidai.

Alidai baada ya hapo, walibeba kichwa na miguu na walishauriana waviweke nyumbani kwake (kwa Bw. Mawe) wasubiri wateja hao ambao walikuwa wakiwasiliana nao kutoka Mwanza mjini, Lamadi na Kahama

Mkuu wa Polisi wilayani Bariadi, Mrakibu wa Polisi, Bw. Paul Kasabago, akiwa eneo la tukio alisema kupatikana kwa viungo hivyo kumetokana na ushirikiano mkubwa wa wanakijiji hicho ambao aliwashukuru kwa kuonesha ushirikiano wa dhati na ulizi shirikishi.

Aliwataja wanaoshukiwa na Polisi kuhusika katika tukio hilo kuwa ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Chenyenye Kishiwa (64), Bw. Sayi Gamanya (47), Bw. Gumbu Nzige (48), Bw. Mboji Mawe (48), Bw. Sayi Mafize (32) na Bw. Salum Mshamamba (52). Wote ni wakazi wa Mkingwabie.

Naye Anneth Kagenda anaripoti kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Walemavu la Haki za Kisheria na Maendeleo, Bw. Gidion Mandesi, jana jijini Dar es Salaam alisema Serikali imeshindwa kudhibiti mauaji ya albino yanayoendelea.

"Serikali inataka kutuambia imani za kishirikina zimeanza wakati huu, mbona hata zamani zilikuwapo na (albino) walikuwepo mpaka wamezeeka hawa kuuawa kama ilivyo sasa," alisema Bw. Mandesi.

Bw. Mandesi alishauri serikali itumie raslimali zake kuwakusanya maalbino na waganga wa jadi, ili wajadili jinsi ya kukomesha mauaji hayo.

Naye Gladness Mboma, anaripoti kuwa Kitengo cha Makosa Dhidi ya Wanadamu kimewanasa zaidi ya watu 57 wakiwemo waganga wa jadi, wafanyabiashara wa madini na wavuvi na kuwafungulia mashtaka ya kuhusika na mauaji ya albino katika maeneo mbalimbali nchini.

Mdhibiti Mkuu wa Kitengo hicho, Bibi. Sidney Mkumbi, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akiojiwa katika kipindi cha kipima joto kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Bi. Mkumbi alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa sita baada ya polisi kufanya msako mkali dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo na kwamba wengi wa watuhumiwa hao wanatoka katika mikoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mara, Kigoma, Kagera na Mbeya.

"Watu wengi wanadhani sisi hatufanyi kazi dhidi ya matukio haya ya kikatili, juhudi zipo na mafanikio yake ni kukamatwa kwa watu zaidi ya 57 wakiwemo wafanyabiashara 13 miongoni mwao watano walikutwa na viungo vya binadamu ambavyo havijathibitishwa kama ni vya albino au la," alisema.

Source:Majira



0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2009 Bloggerized by : CTU | Inspired By ReedzSolution : ReedzSolution