Serikali yawakemea Mengi na Rostam
SERIKALI imetoa tamko rasmi kubeza malumbano yaliyoibuka hivi karibuni kati ya Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na mfanyabiashara mwenzake, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, alisema serikali inawataka Mengi na Rostam, kuacha mara moja malumbano yao kupitia vyombo vyao vya habari wanavyovimiliki na badala yake wawasilishe madai na vielelezo vyao kwa mamlaka husika ili hatua zinazofaa zichukuliwe.
Akisoma tamko hilo lililosainiwa na Waziri wa wizara hiyo, Kapteni mstaafu George Mkuchika, aliyeko Busanda, wilayani Geita, mkoani Mwanza, kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mdogo, alisema uchunguzi walioufanya na vyombo vya dola, umebaini kuwa Rostam na Mengi, wamekiuka sheria kwa kutumia vyombo vyao vibaya na wanaweza kuligawa taifa.
“Serikali imetafakari kwa makini malumbano ya wafanyabiashara hawa na kubaini kuwa wanalipeleka taifa pabaya, kwani malumbano yao yanaweza kuligawa taifa na kutishia uvunjifu wa amani, kama yataachwa yaendelee.
“Serikali imebaini kuwa malumbano ya Mengi na Rostam, yamewagawa wananchi katika makundi mawili, ya wale wanaounga mkono kauli za Rostam na wanaomuunga mkono Mengi,” alisema Naibu Waziri Bendera.
Bendera alienda mbali kwa kusema kuwa malumbano hayo, yamesababisha kuwapo kwa matumizi mabaya ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Mengi (redio, magazeti na televisheni), na Rostam, ametumia vibaya magazeti yake, kwa manufaa binafsi, kinyume cha maelekezo ya sera ya habari na utangazaji ya mwaka 2003.
“Sera ya habari ya mwaka 2003, imekataza chombo cha habari kutumika kwa manufaa binafsi ya mmiliki au mtendaji, bali kitumike kwa manufaa ya umma, chombo cha habari kiongozwe na maadili ya taaluma na jamii husika na chombo cha habari kisitangaze habari kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, kabila, dini, jinsia, au ulemavu au kuchochea uhasama.
“Kwa hali hiyo, malumbano ya Rostam na Mengi yakiachwa yaendelee, yanaweza kulitumbukiza taifa pabaya katika uvunjaji wa amani,” alisema.
Alionya kuwa serikali haitakubali kusikia malumbano ya Rostam na Mengi, ambayo yanaweza kuhatarisha hali ya utulivu na amani nchini yakiendelea bila sababu za msingi.
“Serikali pia haitavumilia kuona vyombo vya habari nchini vikichangia kuligawa taifa katika makundi na kudumaza maendeleo,” alisema.
Aliwataka Rostam na Mengi, kukumbuka kuwa malumbano yao kwa kutumia vyombo vyao vya habari na wakati mwingine kuonekana kana kwamba wanalihutubia taifa, ni kutowatendea haki watu wengine ama kampuni au mashirika ambayo yametajwa katika malumbano hayo lakini hawana vyombo binafsi.
“Hawa wengine wameonewa, hawana vyombo vya habari, unanitaja mimi Bendera, sina gazeti, nitatumia nini kuzungumzia? Nitajielezea wapi kama walivyotumia Rostam na Mengi?” alihoji Bendera.
Naibu waziri huyo alizidi kueleza kuwa serikali inasikitishwa na kitendo cha Mengi cha kuzungumzia kesi ambazo tayari zipo mahakamani wakati sheria za nchi zinakataza mtu, watu, kuzungumzia ama kujadili suala ambalo lipo mahakamani, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwahukumu na kuwatia hatiani wahusika bila wao kupewa fursa ya kujitetea au kusikilizwa.
“Serikali inawataka wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini katika kutimiza wajibu wao kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao badala ya kuandika au kutangaza kulingana na matakwa ya wamiliki wa chombo husika,” alisema.
Hata hivyo Naibu Waziri hakuweza kujibu maswali ya wanahabari kwani kila alipoulizwa swali, alitoa majibu ya mkato na kudai kuwa huo ndio msimamo wa serikali na taarifa yake inajitosheleza.
“Hii taarifa ni msahafu tosha, kila kitu kipo hapa, someni mstari kwa msitari, tumefanya uchunguzi wa kitaalamu,” alianza kuwaeleza waandishi wa habari kabla ya kuuliza maswali.
Alipoulizwa kuhusu uhalali wa Televisheni ya Taifa (TBC1) kurusha kipindi maalumu cha Rostam, wakati alitumia nafasi hiyo pia kumsema Mengi kwamba alitumia kituo chake cha ITV vibaya, Bendera aliruka kwa kusema hiyo si kazi yake, bali ya Bodi ya TBC1 na ndio wanaopaswa kuulizwa na kujibu swali hilo.
“Mimi si msemaji wa TBC1, kuna Tido na bodi yake, kawaulize kama Rostam alikuwa sahihi au alikosea,” alisema waziri huyo kwa ufupi.
Alienda mbali zaidi na kusema kuwa kuanzia sasa serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa vyombo vya habari ambao hawatazingatia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na sheria ya utangazaji ya mwaka 2003 katika kutekeleza kazi zao za kukusanya na kusambaza habari.
Alipoulizwa ni kwanini serikali isitunge sheria ya kukataza viongozi wa umma, kama wabunge kumiliki vyombo vya habari, alisema serikali haijachelewa bado kwani inaweza kufanya hivyo ikiona inafaa.
Tamko hilo la serikali kupitia wizara hiyo limekuja wakati yalishatolewa matamko mengine mawili kwa nyakati tofauti na viongozi wa juu wa serikali.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikwisha kutoa msimamo wa serikali alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo mjini Dodoma wakati wa mkutano wa 15, akiwataka waliokashifiwa na Mengi kwenda mahakamani, huku vyombo husika vikichunguza tuhuma hizo.
Mbali na Pinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba, alishatoa msimamo wa serikali, kwa kusema Mengi amechemka kuwataja wenzake mafisadi papa, kwani hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Hata hivyo, Waziri Bendera alisema kauli aliyoitoa ndio msimamo unaotambuliwa na serikali na si vinginevyo.
“Nimesema, msemaji wa serikali ni mimi, wizara yangu ndiyo yenye mamlaka ya kuzungumzia lolote linaloigusa serikali, taarifa yangu ndiyo inayopaswa kuzingatiwa,” alisema huku akionyesha karatasi zake juu na kuongeza kuwa:
“Hii ndiyo taarifa ya serikali, waziri wangu yupo makini, tunakwenda kwa data (takwimu), tuna watu weledi na wataalamu, vingine hatuvitambui,” alisema.
Pia naibu waziri hakuweza kuwaeleza wanahabari sababu za kuzungumzia suala hilo, hasa la kuchafuana kati ya wafanyabiashara hao wawili, wakati tayari walishapelekana mahakamani kwa kesi hiyo hiyo, na kudai kuwa serikali haikurupuki na haijachelewa kutoa tamko lake.
“Serikali haikurupuki, na haifanyi kazi kwa kuendeshwa na watu, haijachelewa kutoa tamko hili,” alisema naibu waziri bila kufafanua.
Aidha, swali jingine ambalo waziri hakutaka kulijibu ni lile lililohusu tuhuma za ufisadi zilizowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilibrod Slaa, aliyetaja majina ya watu 11, mwaka 2007.
Swali hilo lilitaka kujua kwanini serikali haikutoa tamko badala yake ikawachunguza kimya kimya watuhumiwa na baadhi yao kufikishwa mahakamani, lakini kwanini tuhuma alizotoa Mengi zinapaswa kutolewa vielelezo na ushahidi?
Tuachane na mambo ya zamani, tuangalie yaliyopo leo,” alimalizia Waziri Bendera na kuondoka huku waandishi wa habari wakinung’unika kwa baadhi ya maswali yao ya msingi kutopewa majibu ya kuridhisha.
Wakati serikali ikitoa tamko lake jana, tayari Mengi amekwisha kumshitaki Rostam kwa kumkashifu, akitaka amlipe sh bilioni 10, huku Rostam akiwa amepeleka vielelezo vyake dhidi ya Mengi katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakati Manji amekimbilia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mahakama ya Kisutu, akilalamika kukashifiwa na anadai kulipwa fidia ya sh moja.
Naibu waziri alihitimisha kwa kusema kuwa serikali kwa mara nyingine inasisitiza kuwa malumbano dhidi ya ufisadi na vitendo vya rushwa bado yanaendelea na inawahimiza wananchi wenye taarifa za vitendo kama hivyo watoe taarifa kwenye vyombo vya dola.
Malumbano hayo yalianza pale Mengi alipoitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwataja wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia kuwa ni ‘mafisadi papa’, wanaolifilisi taifa.
Mengi aliwatuhumu wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia, Jeet Patel, Rostam Aziz, Yusuf Manji, Subhash Patel, na Tanil Sumaiya kuwa ni mafisadi papa wanaoliibia taifa mabilioni ya fedha.
Mbunge wa Igunga, Rostam, ndiye alikuwa wa kwanza kujibu tuhuma hizo, lakini naye alimtuhumu Mengi kuwa ni fisadi nyangumi kwa kumhusisha na kukopa fedha za Mpango wa Kusaidia Wafanyabiashara - Commodity Import Support (CIS).
Juzi mfanyabiashara mwingine Shubhash Patel, aliyetuhumiwa na Mengi kuwa miongoni mwa mafisadi papa, alijitokeza na kudai kuwa Mengi amemkashifu, lakini hajaamua endapo atakwenda mahakamani.
Source: Tanzania Daima
Lupe Fiasco fears Mount Kilimanjaro Climb
In an effort to bring awareness to the worldwide water crisis, Chicago lyricist Lupe Fiasco has confirmed plans to ascend Tanzania’s Mount Kilimanjaro. Fiasco was recruited for the stunt by Ethiopian pop singer Kenna, whose father nearly perished as a child due to a lack of clean drinking water.
“My dad almost died as a child from waterborne diseases in Ethiopia, and he had talked to me about digging a well there,” Kenna explained to Elle Magazine. “I thought, 'I have too many friends who would be concerned with the subject of clean water.’ Maybe I can help out.”
Mount Kilimanjaro boasts the highest peak on the African continent at 19, 330 feet. Most routes to the top of the mountain take a maximum of 6 to 7 days. Although the voyage is a popular retreat amongst climbers, the journey is not without its dangers.
An estimated 10 people die every year attempting to climb Kilimanjaro. The majority of the fatalities are due to altitude sickness, which can cause swelling of the brain tissue (high altitude cerebral edema).
Despite the risks for a novice climber, Fiasco plans to make the event a light-hearted competition with his friend Kenna. “I'm an adventure junkie,” Fiasco stated. “Part of the motivation is beating Kenna to the top. Sabotaging his tent, taking the lining out of his coat, [and] lacing it with ants or something like that.”
Along with Kenna and Fiasco, pop superstar Justin Timberlake is expected to participate. The Mount Kilimanjaro charity climb is scheduled to take place this Fall.
At press time, Lupe’s anticipated third studio album Lasers is due out in June 2009.
Source: SwahiliRemix
'Muuaji' asimulia walivyomchinja albino
JESHI la Polisi wilayani Bariadi mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na wanannchi wa kijiji cha Mkingwabie, wamefanikiwa kukamata kichwa na miguu miwili iliyonyofolewa kwenye mwili wa albino, Bw. Lyaku Nkanyabilu (50), aliyeuawa kikatili mjini hapo na kuzikwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Viungo hivyo vilipatikana jana nyumbani kwa Bw. Mbonje Mawe (41), mkazi wa kijiji hicho na Majira ilishuhudia polisi wakishirikiana na wananchi kufukua kichwa cha marehemu Nkanyabilu nyumbani kwa mtuhumiwa wa mauaji.
Baada ya kufukuliwa kichwa hicho, Bw. Mawe aliongoza kundi la polisi na wananchi hao kwenda sehemu iliyokuwa imefukiwa miguu ya albino huyo ambapo ilifukuliwa ikiwa imefungwa na gunia.
Bw. Mawe alikiri kushiriki mauaji hayo na kuwataja wenzake sita anaodai kushirikiana nao, akiwemo Mwenyekiti wa kijiji hicho, pamoja na wenyeviti wawili wa vitongoji. Alisema walikuwa na nia ya kuuza viungo hivyo kwa wateja ambao walikuwa wakiwasiliana.
Akisimulia tukio zima lilivyokuwa, Bw. Mawe alidai siku ya tukio akiwa na wenzake sita, walipanga kumuua Bw. Nkanyabilu kwa kushirikiana na shemeji yake, Bw. Sayi Gamani.
Alidai Bw. Gamani alimdanganya Bw. Nkanyabilu kuwa anampeleka hospitali kumtibu maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kabla ya kushirikiana kumkamata na kwenda kumuua.
"Ilipofika saa saba usiku, tulimkamata Bw. Lyaku (Nkanyabilu) na kumpeleka mtoni, tulipofika huko tulimlazimisha kuingiza kichwa kwenye maji hadi alipokufa, tukamchinja, tukamkata miguu na baada ya hapo, tukaiingiza viungo hivyo kwenye gunia moja na mwili wake kwenye gunia lingine na kutumbukiza mwili wake kwenye maji," alidai.
Alidai baada ya hapo, walibeba kichwa na miguu na walishauriana waviweke nyumbani kwake (kwa Bw. Mawe) wasubiri wateja hao ambao walikuwa wakiwasiliana nao kutoka Mwanza mjini, Lamadi na Kahama
Mkuu wa Polisi wilayani Bariadi, Mrakibu wa Polisi, Bw. Paul Kasabago, akiwa eneo la tukio alisema kupatikana kwa viungo hivyo kumetokana na ushirikiano mkubwa wa wanakijiji hicho ambao aliwashukuru kwa kuonesha ushirikiano wa dhati na ulizi shirikishi.
Aliwataja wanaoshukiwa na Polisi kuhusika katika tukio hilo kuwa ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Chenyenye Kishiwa (64), Bw. Sayi Gamanya (47), Bw. Gumbu Nzige (48), Bw. Mboji Mawe (48), Bw. Sayi Mafize (32) na Bw. Salum Mshamamba (52). Wote ni wakazi wa Mkingwabie.
Naye Anneth Kagenda anaripoti kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Walemavu la Haki za Kisheria na Maendeleo, Bw. Gidion Mandesi, jana jijini Dar es Salaam alisema Serikali imeshindwa kudhibiti mauaji ya albino yanayoendelea.
"Serikali inataka kutuambia imani za kishirikina zimeanza wakati huu, mbona hata zamani zilikuwapo na (albino) walikuwepo mpaka wamezeeka hawa kuuawa kama ilivyo sasa," alisema Bw. Mandesi.
Bw. Mandesi alishauri serikali itumie raslimali zake kuwakusanya maalbino na waganga wa jadi, ili wajadili jinsi ya kukomesha mauaji hayo.
Naye Gladness Mboma, anaripoti kuwa Kitengo cha Makosa Dhidi ya Wanadamu kimewanasa zaidi ya watu 57 wakiwemo waganga wa jadi, wafanyabiashara wa madini na wavuvi na kuwafungulia mashtaka ya kuhusika na mauaji ya albino katika maeneo mbalimbali nchini.
Mdhibiti Mkuu wa Kitengo hicho, Bibi. Sidney Mkumbi, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akiojiwa katika kipindi cha kipima joto kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.
Bi. Mkumbi alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa sita baada ya polisi kufanya msako mkali dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo na kwamba wengi wa watuhumiwa hao wanatoka katika mikoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mara, Kigoma, Kagera na Mbeya.
"Watu wengi wanadhani sisi hatufanyi kazi dhidi ya matukio haya ya kikatili, juhudi zipo na mafanikio yake ni kukamatwa kwa watu zaidi ya 57 wakiwemo wafanyabiashara 13 miongoni mwao watano walikutwa na viungo vya binadamu ambavyo havijathibitishwa kama ni vya albino au la," alisema.
Source:Majira
Arsenal Charii!, Yabugizwa 4-1 na Chelsea Emirates.
Timu ya Arsenal imepewa kipigo cha nguvu ambacho hawakukitegemea toka kwa Chelsea kwenye uwanja wao wa Emirates baada ya kukubali kubugia magoli 4-1.
Timu zote mbili ziliingia uwanjani leo zikiwa na majeraha ya kutupwa nje ya kombe la mabingwa wa ulaya katikati ya wiki iliyopita.
Uzoefu katika soka ulidhirika kuwa ni muhimu sana baada ya vijana wa Arsene Wenger kutawala dakika zote 45 za kipindi cha kwanza lakini mwishoni mwa kipindi hicho Arsenal ilikuwa tayari imeishabugia mabao mawili.
Chelsea waliwashtua wenyeji wao kwa mabao mawili ya haraka haraka katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Alex na Kolo Toure na kuifanya Chelsea iende mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.
Dakika nne baada ya kuanza kwa kipindi cha pili jahazi la Arsenal lilizidi kuzama baada ya beki wake Kolo Toure kuizawadia Chelsea goli la tatu katika dakika ya 49 kwa kuuzamisha nyavuni kwake mpira wa krosi iliyochongwa na Asheley Cole.
Nicklas Bendtner aliifungia Arsenal goli la kufutia machozi katika dakika ya 70 kabla ya Malouda kuhitimisha karamu ya magoli ya Chelsea katika dakika ya 86.
Chelsea kwa ushindi wa leo imejihakikishia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ya Uingereza.
Katika mechi nyingine iliyochezwa leo, Manchester United imekinyakua tena kiti chake cha uongozi wa ligi baada ya kuwagaragaza mahasimu wao Manchester City kwa mabao 2-0.
Baada ya Kumtosa Chris Brown, Rihanna Amrudia Mpenzi wake wa Utotoni.
Rihanna mwenye umri wa miaka 21 alikuwa akitoka na Negus Sealy ambaye sasa ana umri wa miaka 24 kabla hajamtosa alipokuwa maarufu.
Taarifa za udaku zilisema kwamba wapenzi hao wa zamani wameamua kuyakumbukia mapenzi yao baada ya Rihanna kuachana na Chris Brown ambaye alimshambulia.
Sealy ametajwa kama ndiye mtu anayemliwaza Rihana na kuwa bega la kulilia la Rihanna baada ya kuvunjwa moyo wake na Chris Brown ambaye alimshambulia na kumjeruhi usoni.
Chanzo hicho cha udaku kililiambia gazeti la News of the World la Uingereza: 'Sealy ndio sehemu ya kujiliwaza ya Rihanna, ni kijana mtanashati, mwenye busara na mpole".
"Mademu wote wanamzimia na kumuita 'mtaalamu wa mapenzi' alikuwa akionekana na Rihanna kabla Rihanna hajawa maarufu".
Wapenzi hao walionekana wakila raha katika ufukwe mmoja katika kisiwa cha Barbados ambapo Rihanna alikuwa amevaa bikini nyeusi na kofia vilivyomkaa vilivyo na kumfanya aonekane 'Hot'.
Rihanna inasemekana kwa jinsi alivyojitosa mzima mzima kwa Sealy huwaambia rafiki zake na familia yake kwamba mapenzi yake na Chris Brown yatabakia kuwa historia.
Chris Brown alipandishwa kizimbani jijini Los Angeles mwezi na alikataa madai ya kufanya shambulizi, akipatikana na hatia anaweza akapewa kifungo cha hadi miaka mitano jela.